Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, ujumbe kamili wa rambirambi uliotolewa na Ayatullah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, kufuatia kifo cha Ayatullah Wahid Khorasani, unasomeka kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na hakika kwake Yeye tutarejea.
Imam Jaafar Sadiq (as) amesema:
“Anapofariki muumini ambaye ni faqihi, pengo hutokea katika Uislamu ambalo hakuna kitu kinachoweza kuliziba.”
Kwa huzuni na masikitiko makubwa, ninatoa rambirambi zangu kufuatia kufariki mwalimu wetu mtukufu, Ayatullah Al-Udhma Hajj Sheikh Hussein Wahid Khorasani (Mwenyezi Mungu autakase utukufu wa roho yake), kwa Mtukufu Wali Al-Asr (roho zetu ziwe fidia kwake), Maraji' wakuu wa Taqalidi (Mwenyezi Mungu aendeleze baraka zao), Kiongozi Mkuu (Mwenyezi Mungu aendeleze kivuli chake), Hawza za kielimu, viongozi na wanazuoni wa dini, taifa kubwa la Iran, wananchi watukufu wa Qum, Waislamu wa dunia nzima, wafuasi wa kizazi cha Mtume Mkuu (s.a.w.w.), wapenzi wa Maraji' na taasisi za Maraji' nchini Iran na duniani kote, taasisi zote za juu za kielimu na za Hawza, na hasa wanawe watukufu pamoja na familia yake tukufu.
Aidha, ninatangaza kusimamishwa masomo katika Hawza za kielimu kuanzia leo hadi mwisho wa wiki hii, ili kutoa heshima kwa hadhi tukufu ya Maraji' na kushiriki katika shughuli za mazishi, maziko na vikao vya maombolezo.
Faqihi huyo mwenye hadhi ya juu na Marjaia mwenye thamani kubwa alitumia takribani karne moja ya maisha yake yenye baraka katika kutafuta elimu, kufundisha, kufanya utafiti, kulea wanafunzi wengi, kuandika na kuzalisha kazi pamoja na nadharia za kielimu, na kuwaongoza na kuwaelekeza wananchi pamoja na wanahawza. Alikuwa sababu ya kukua na kuimarika Hawza ya kielimu ya Qum na Hawza nyingine, sambamba na kuendeleza tafiti katika fani za Fiqhi, Usulul-Fiqhi, Tafsiri ya Qur’an, Historia na elimu nyingine za Kiislamu.
Faqihi huyo mtafiti wa Hawza alibahatika kuifahamu Hawza ya kale ya Najaf Ashraf na kunufaika na elimu ya wanazuoni wake mashuhuri. Baadaye alifundisha katika Hawza tukufu ya Mashhad, kisha akatulia katika Hawza ya kale na yenye heshima ya Qum. Kupitia fikra zake za kina, tafiti zake za undani, maelezo yake yenye mvuto na hamasa, pamoja na vikao vyake vya ufundishaji vilivyokuwa na mahudhurio makubwa, alipanua mipaka ya elimu za Fiqhi, Usulul-Fiqhi na Tafsiri, akalea wanafunzi wengi sana na kufungua upeo mpya katika elimu za Kiislamu.
Mti huo mkubwa na imara wa elimu ya Fiqhi ulikuwa uking’ara kama jua katika vikao vyake vya mijadala na mafundisho, mikusanyiko yake yenye manufaa ya mijadala ya kielimu, tafiti na uchunguzi wa kina wa masuala ya Fiqhi, pamoja na fikra zake nyeti katika elimu ya Kalam, Historia na nyanja nyingine. Vilevile, katika nafasi yake ya kutoa hotuba za Imam Husseini (as), kuwaongoza na kuwaelekeza wananchi nchini Iran na katika nchi nyingine, aliacha kumbukumbu na baraka nyingi.
Mwalimu huyo mtukufu alikuwa miongoni mwa watetezi wa Uislamu wetu adhimu, Wilaya ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume (s.a.w.w.), pamoja na vyeo na hadhi tukufu za Imam Ali (as) na Bibi Fatimah (as). Katika kipindi cha mapambano ya wananchi wa Iran na Mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amnyanyulie daraja lake tukufu), na baadaye katika zama za Kiongozi Shahidi, Imam Khamenei (Mwenyezi Mungu amfunike kwa rehema Zake), alikuwa pamoja na Mapinduzi ya Kiislamu. Alikuwa na moyo wa kujali, akitoa mwongozo na nasaha kwa wananchi wa Iran, Hawza za kielimu na mfumo wa Kiislamu.
Vilevile, uungaji mkono wake katika kukuza elimu na maadili mema ndani ya Hawza na jamii, pamoja na juhudi zake za kuwalea wanafunzi na wanazuoni wenye uwezo na vipaji vya hali ya juu, na kuanzisha vituo na vitengo maalumu vya masomo ya kitaalamu, ni mambo yanayostahili kusifiwa.
Zaidi ya yote hayo, hali yake ya kiroho, usafi wa moyo, tabia njema, kujitenga na anasa za dunia, maisha yake ya kujisitiri na kujiheshimu, kushikamana kwake na mila halisi za kimaadili na kielimu za Hawza, pamoja na mapenzi yake kwa Mtukufu Wali Al-Asr (roho zetu ziwe fidia kwake), vitaendelea kuwa chanzo cha msukumo kwa Hawza, vyuo vikuu, wanafunzi wa dini, vijana na walimu.
Na sasa, nguzo hii kubwa ya elimu ya Fiqhi imepaa kuelekea ulimwengu wa juu, na kuziacha Hawza za kielimu, wanafunzi wake na wapenzi wake katika maombolezo. Kwa sasa, kilichobaki ni Hawza za kielimu, wanafunzi wake vijana na walimu wake wapendwa, pamoja na urithi wake mkubwa wa kielimu. Ahadi yetu sote ni kuendeleza njia ya utakaso, elimu ya Fiqhi na Marjaa, na kuendelea kufuata njia ya Uislamu, mafundisho ya madhehebu haya, Mapinduzi ya Kiislamu na mashahidi wetu watukufu.
Pamoja na kuisalimia roho yake safi, tunatumaini kuwa Hawza za kielimu, wananchi watukufu wa Qum, Iran na dunia nzima, zitatimiza wajibu wao kwake na kwa madhehebu ya Ahlul-Bayt (amani iwe juu yao), kwa kushiriki kwa wingi katika shughuli zote za maombolezo na kumbukumbu zitakazofanyika kwa heshima yake.
Aliishi maisha yenye furaha na akafariki akiwa na furaha.
Alireza Arafi
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran
Maoni yako